CAF yawapitisha wanne wapya Yanga..


Shirikishi la Soka Afrika (CAF), limepitisha majina ya wachezaji wanne wapya wa Yanga, kipa Benno David Kakolanya, Hassan Hamisi Ramadhan ‘Kessy’, Vincent Andrew Chikupe na Juma Hassan Mahadhi kucheza Kombe la Shirikisho.

Yanga inafungua dimba na MO Bejaia Juni 19, mwaka huu, Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria na sasa wanne hao wako huru kucheza.

Yanga ambayo imeweka kambi katika hoteli ya Rui mjini Antalya, Uturuki tangu Jumapili na itaondoka kesho kwenda Bejaia kwa ajili ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu.

Hassan-Kessy-Yanga-Bongosoka

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas Mapunda amesema kwamba wametumiwa leseni za wachezaji hao kutoka CAF.

“CAF imetuma leseni za wachezaji hao wanne wapya wa Yanga na maana yake sasa wako huru kucheza Kombe la Shirikisho,”amesema Mapunda.

Kakolanya amesajiliwa kutoka Prisons ya Mbeya, wakati Kessy ametoka kwa mahasimu, Simba, Vincent ametoka Mtibwa Sugar na Mahadhi ametoka Coastal Union.

Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.

Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com