Chanzo mgongano wa viongozi Yanga hiki hapa…


Siku ya jana jumla ya viongozi watano (5) wa klabu ya soka ya Yanga, walitoka katika nafasi zao. Kati ya hao watatu ilikuwa ni kwa kujiuzulu na wawili ilikuwa ni kwa kusimamishwa na kamati ya utendaji ya klabu hiyo ikiwa kama hatua ya kinidhamu.

Waliosimamishwa…

Kupitia barua ya tarehe 27 Machi, 2020 ya mwenyekiti wa Yanga, Dkt Mbette Mshindo Msolla viongozi ambao wamechukuliwa maamuzi ya kusimamishwa nafasi zao ni wajumbe wawili wa kamati ya utendaji.

Wajumbe hao ni Salum Rupia na Frank Kamugisha huku barua hiyo ikieleza kuwa, kamati ya utendaji imechukua maamuzi hayo ikiwa ni hatua za kinidhamu juu yao.

Waliojiuzulu…

Barua ya kuwasimamisha wajumbe hao wawili ilikuja mara baada ya wajumbe wa tatu wa kamati ya utendaji kuandika barua ya kujiuzulu nyadhfa zao.

Wajumbe hao ni Rogers Gumbo, Shija Richard, na Said Kambi.

Shija Richard

Kauli tata za waliojiuzulu…

Shija Richard, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, alinukuliwa katika barua yake akisema kuwa Yanga ni kubwa kuliko yeye au mtu yoyote na hata zungumza chochote juu ya yaliyosemwa.

” Ukweli hata usipousema, huwa unatabia ya kujitokeza wenyewe japo taratibu, lakini huwa unadumu milele ” aliongeza Shija.

Kauli hii imezua utata mkubwa juu ya kinachoendelea klabuni hapo hasa kutokana na kufanana na ile ya Rogers Gumbo aliyeandika, ” Sitazungumza chochote ila naamini ipo siku ukweli utajulikana,” alieleza Gumbo katika barua yake.

Chanzo ni GSM na mabadiliko…

Barua ya klabu ya soka ya Yanga, imeeleza kuwa kwa wajumbe waliosimamishwa nafasi zao ni baada ya kuwepo kwa sintofahamu iliyopelekea mdhamini wa klabu hiyo GSM, kujitoa katika majukumu yasiyo ya kimkataba.

Jambo hili limeungwa mkono na mmoja wa wanachama wa klabu hiyo, Juma Mohamed ambaye kupitia barua yake kwa mwenyekiti, Dkt Msolla aliweka wazi kuwa kuna watu ambao wana nia ya kukwamisha hatua za mabadiliko ndani ya klabu, kutoka umiliki wa wanachama mpaka kampuni na kuwa mfumo wa hisa.

“Mgongano wa kimaslahi ndani ya timu, ndio unaopelekea utofauti wa fikra na mgongano wa mawazo hali inayoleta kutokuelewana huko baina ya viongozi,” alieleza Hussein Msoleka, mchambuzi wa masuala ya kimichezo nchini.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com