Hatimaye Simba wa kimataifa , wabeba kombe la shirikisho…


Hatimaye klabu ya wekundu wa msimbazi , Simba imefanikiwa kushiriki mashindano ya kimataifa baada ya kufanikiwa kuilaza timu ngumu ya Mbao FC , goli 2 -1 katika mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho uliopigwa katika uwanja wa Jamhuri , Dodoma .

Ubingwa walioupata Simba unakata kiu ya miaka minne klabuni hapo kwenye ushiriki wa mashindano ya kimataifa huku  mara ya mwisho kushiriki ikiwa ni  mwaka 2013 walipotolewa  na Recreativo de Lobolo ya Angola .

Katika mchezo wa leo , kipindi cha kwanza kilianza kwa presha kubwa huku uwanja wa Jamhuri ukiwa umejaa mashabiki .

Dakika ya 10 ya mchezo , Mshambuliaji wa Simba Laudit Mavugo alikosa nafasi ya wazi ya bao baada ya kubaki na kipa na kupiga shuti lililotoka nje . Mchezo uliendelea huku kila timu ikishambulia na mpira ukichezwa hasa katikati ya uwanja . Hadi kipindi cha kwanza kinaisha hakuna timu iliyokua imeona lango la mwenzake .

Kipindi cha pili  kilianza kwa kasi lakini milango ya kila timu iliendelea kuwa migumu hadi dakika 90 zinamalizika hali iliyopelekea kuongezwa dakika 30 .

Katika dakika 30 za nyongeza ndio kila timu iliweza kuchacharuka na kuanza kutafuta bao la mwenzie kwa udi na uvumba .

Mabadiliko aliyofanya  kocha wa Simba , Joseph Omog ya kumtoa Said Ndemla dakika 83 na kumuingiza Fredrick Blagnon yaliweza kuzaa matunda katika dakika ya 95 ya mchezo baada ya  Simba kupata bao la kuongoza kupitia kwa Frederic Blagnon akipokea pasi ndefu kutoka kwa Abdi Banda, beki wa Mbao akafanya uzembe, ikampita, Blagnon akatuliza, akapisha shuti kali na mpira kujaa wavuni.

Dakika ya 109 ,  Mbao FC walifanikiwa kupata bao la kusawazisha  kutokana na uzembe wa  mabeki wa Simba baada ya kupigwa  mpira mrefu huku mabeki wakijua Robert Ndaki wa Mbao FC ameotea, anabaki na kipa kisha anamchambua vizuri na kuandika bao la kusawazishia .

Dakika ya 118 ya mchezo , Simba waliweza kupata penati baada ya mchezaji wa Mbao FC kuunawa mpira ndani ya box .  Shiza Kichuya anapiga penati nzuri inayoifanya Simba SC kujipatia bao la pili na la ushindi . Dakika ya 123 , Mwamuzi anapuliza kipenga kuashiria mpira kuisha na ushindi kwa simba FC .

Ukiachana na ubingwa wa leo na tiketi ya kushiriki michuano ya kombe la shirikisho Afrika , Simba pia imejinyakulia kitita cha  Sh. Milioni 50 kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo , Azam TV.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com