Je , Simba kulipa kisasi cha Mtibwa leo kwenye ligi kuu?


BAADA ya kusimama kwa takribani wiki mbili, Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea tena leo, huku Simba ikijaribu kulipa kisasi dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba itataka kulipa kisasi cha kufungwa na Mtibwa bao 1-0 na kuondolewa katika michuano ya Mapinduzi mjini Zanzibar na kupelekea kutimuliwa kwa kocha wake Muingereza Dylan Kerr.Timu hiyo kwa sasa iko chini ya kocha mpya Mganda Jackson Mayanja aliyewahi kuifundisha Kagera Sugar kabla ya kwenda Coastal Union na kutimuliwa msimu huu.

Simba-Mapinduzi-cup

Mayanja alikaririwa juzi akisema kuwa Mtibwa ni timu ya kawaida tu na wanatarajia kuibuka na ushindi, huku akiomba wapenzi wa timu hiyo kuwaunga mkono. Katika mchezo mwingine leo, vinara wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 , Azam FC wenyewe watakuwa wenyeji wa African Sports katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wao wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Azam FC inaoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 35 baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 33, ambapo imepania kushinda mechi hiyo ili kuzidi kujichimbia kileleni wakati Yanga wakicheza kesho Jumapili dhidi ya Ndanda FC.

Mechi zingine za ligi hiyo leo ni kati ya JKT Ruvu na Mgambo JKT Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Toto Africans na Prisons Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Stand United na Kagera Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Mbeya City watakuwa wenyeji wa Mwadui FC ya Shinyanga katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya huku Coastal Union na Majimaji zikitifuana kwenye Uwanja wa Uwanja wa Majimaji, Songea.

Ligi Kuu itaendelea tena Jumapili kwa mechi moja tu, wakati mabingwa watetezi Yanga wakiikaribisha Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Baada ya mechi za leo na kesho, ligi hiyo itakuwa imebakisha mchezo mmoja ili kumalizika kwa duru la kwanza baada ya timu zote kuwa zimecheza mechi 15.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com