John Bocco: Tunaenda zanzibar kubeba kombe la Mapinduzi…


Nahodha  wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’ amesema wanakwenda Zanzibar kwa lengo moja kubwa, kubeba Kombe la Mapinduzi.

Bocco alisema wao kama wachezaji wamekubaliana kwenda kubeba Kombe. “Mashindano ya Mapinduzi si mageni kwa Azam FC, michuano hiyo si myepesi ni migumu, sisi kama wachezaji tunaenda kushindana, naamini ni sehemu moja ya msimu huu, hivyo tukiweza kuchukua kombe itakuwa ni faraja kwa klabu na mashabiki wetu pamoja na sisi wachezaji.

“Tukitoka huko hata tukirudi kwenye ligi tutakuwa na morali mzuri wa kuendeleza ushindi kwenye ligi, michuano ya FA na Kombe la Shirikisho Afrika,” alimalizia Bocco.

Azam FC inaenda huko ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kulitwaa taji hilo mara mbili mfululizo katika miaka ya 2012 na 2013. Azam itaanza kuwania taji la tatu la Mapinduzi kwa kumenyana na Zimamoto kesho saa 10.15 jioni kabla ya baadaye kucheza na Yanga ya Dar es Salaam na Jamhuri ya Pemba kukamilisha mechi za Kundi B.

Bocco pia amewatakia mashabiki wa timu hiyo heri ya mwaka mpya 2017 na kuwashukuru kwa sapoti yao waliyoionyesha mwaka huu.

“Kwanza tunawashukuru mashabiki wetu kwa uvumilivu waliouonyesha, kwa sapoti waliotupa katika kipindi chote kigumu tulichopitia, kama wachezaji na timu kwa ujumla tunawaomba waendelee kuwa na moyo huo huo na pia tunawatakia kheri ya mwaka mpya (2017) na wamalize mwaka huu vizuri, tuendelee kuwa pamoja ili kuisaidia timu yetu iweze kufanya vizuri,” alisema.

Mbali ya taji la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Cecafa Kagame Cup, Azam pia inajivunia taji la Ngao ya Jamii waliyobeba Agosti 17, mwaka 2016 kwa kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com