Kwanini Mo Dewji anahitaji kuwekeza asilimia 51 Simba?


KLABU ya Simba ya hapa nchini ipo kwenye mchakato wa kupata mwekezaji mpya ambaye amepanga kuinua kiwango cha soka na mapato klabuni hapo. Huyo si mwingine bali ni mdau wa siku nyingi wa soka hapa nchini, Mohammed Dewji ambaye pia ni mkurugenzi wa Kampuni ya MeTL.

Mo Dewji anafahamika kuwa mpenda soka. Amewahi kuzidhamini na kumiliki timu. Amewahi pia kuwa mdhamini mwenye mafanikio katika klabu ya Simba mwaka 2003 ilipocheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Sasa Mo Dewji amerudi tena kwenye anga za soka na sasa anataka kuwekeza klabuni hapo. Kwa mujibu wa gazeti la DIMBA, Dewji anahitaji kuwekeza hisa za asilimia 51 katika klabu ya Simba.

Hebu tujiulize ni kwanini Mo anataka kuwekeza kwa asilimia 51 klabu ya Simba?  Kwakuwa mimi ni mtaalamu wa masuala ya biashara, uchumi na uwekezaji basi ningeanza na kueleza viwango vya uwekezaji (Investment Levels) na kwanini anahitaji asilimia 51 za hisa.

Tunaposema viwango vya uwekezaji katika makampuni mathalani tunajikita sana katika muundo wa umiliki wa kampuni. Mara nyingi kampuni au makampuni humilikiwa na wanahisa (owners of shares).

Kwa lugha nyepesi huwa tunasema wamiliki wa kampuni au muundo wa umiliki wa hisa katika uwekezaji wa kampuni au makampuni hutambuliwa na asilimia ya umiliki katika hisa za kampuni, maana sasa Simba itakuwa imepanua wigo wa kujiendesha kikampuni.

Mohamed-Dewji-SImba

1. Umiliki wa kiwango cha awali

Umiliki wa kiwango cha awali (Ordinary Investment Level), hapa mwekezaji katika aina hii ya uwekezaji huwa ana umiliki wa hisa zisizofika 20% katika kampuni husika.

Maana yake ni kwamba, mwekezaji atakuwa na ushawishi tu katika kampuni husika lakini hatakuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi yoyote yale ikiwepo kudhibiti shughuli kuu ya uendeshaji wa klabu ya Simba.

Hiyo ni kwa mujibu wa sheria ya makampuni ya Tanzania toleo la 2012 ambayo inaendeleza kuwa mwekezaji lazima awe na zaidi ya 50% ya umiliki wa hisa katika kampuni ndipo atakuwa na mamlaka na maamuzi ya kufanya lolote alitakalo. Kwahiyo Mo katika klabu ya Simba ni lazima awekeze kwa asilimia 51 ili kufanya maamuzi kwa sababu umiliki wa hisa zake.

2. Umiliki kiwango cha kati

Mwekezaji ana miliki zaidi ya 20% lakini hazifiki 50% ya umiliki wa hisa katika kampuni. Kwa lugha ya kitaalamu huitwa Associate Investment Level. Hapa ni kwamba mwekezaji humiliki hisa kutoka 20% hadi 49%  katika klabu ya Simba ama kampuni yoyote.

Hali kadhalika aina hii ya uwekezaji tunaona pia kuwa mwekezaji hana maamuzi ya mwisho au hana mamlaka ya kuamua chochote katika kampuni au ndani ya klabu ya Simba, lakini mwekezaji ana ushawishi tu kwa wenye mamlaka.

3. Muungano wa uwekezaji

Kwa lugha ya kitaalamu hutiwa Jouint Venture. Muungano wa wawekezaji, ambao huungana katika kumiliki kampuni na kuiendesha kwa makubaliano maalumu.

Hii huwa si lazima kuangalia mwekezaji mwenye hisa nyingi bali wawekezaji wanaungana kwa makubaliano maalumu ili kuendesha kampuni au makampuni ikiwemo klabu kama ya Simba.

Katika aina hii ya uwekezaji hasa katika hisa makampuni hufanya makubaliano ya pamoja katika kuendesha mamlaka. Kampuni huwa huendeshwa kwa namna walivyokubaliana si uamuzi wa mtu mmoja.

4. Uwekezaji wa kiwango cha juu

Hii kitaalamu huitwa Subsidiary Investment Level. Tunaweza kusema hapa ndipo penye uwekezaji wa kiwango cha juu sana katika kampuni au timu kama ya Simba.

Mwekezaji humiliki zaidi ya 50% za hisa katika kampuni hivyo basi ndiye mwenye maamuzi yote ya uendeshaji. Yeye ndiye mwenye mamlaka yaani mwenye sauti kubwa katika kampuni, au klabu ya Simba kama itampa Mo Dewji.

Mwekezaji huyu ndiye mwenye sauti ya mwisho na ambaye hupata gawio kubwa la mapato ya kampuni au klabu kama Simba. Kingine ni kwamba huyu ndiye mwenye haki ya kuchagua (Voting rights) kwa sababu ana uwezo wa kushawisha na mwenye uwezo kwa kudhibiti shughuli zozote za kampuni.

Hapa mwekezaji huwa anamiliki  hisa zaidi ya 50% ya umiliki wa kampuni pia. Mwekezaji hufanya hayo yote kwa sababu kuu moja, anahitaji faida, uendeshaji rasmi na utaratibu unaoeleweka na kusimamiwa kitaalamu. Hiki ndicho kinachotakiwa klabu ya Simba na wanachama wawe tayari kupoteza baadhi ya maamuzi.

Makala hii imeandikwa na aggreykulwa (+255762345031 /+255713632422)

 

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Bonyeza hapa kupata offer kabampe. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com