Kwanini Simba haitakiwi kumsajili Okwi…..


Klabu ya wekundu wa msimbazi , Simba imetangaza dau la Sh milioni 240 kwa ajili ya kumrejesha mshambuliaji Emmanuel Okwi, ambaye hadi sasa amecheza mechi nne tu katika timu ya SonderjyskE.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Okwi tangu ajiunge na timu hiyo ya Denmark Julai 10 mwaka jana akitokea Simba, amecheza mechi nne za Ligi Kuu nchini humo maarufu kama Danish Sas Ligaen na hajafunga goli hata moja, huku akiwa na kadi moja ya njano.

Ushindani wa namba unamweka benchi baada ya kucheza mechi mbili msimu wa mwaka jana na mbili msimu huu kati ya michezo 16 iliyochezwa kwenye ligi hiyo kwa sasa, ikiwa inashika nafasi ya sita kwenye msimamo na pointi zake 23, huku timu kinara ikiwa ni FC Copenhagen yenye pointi 38, ikifuatiwa na Brondby 32, Midtjyland 29, Randers 29 na Lyngby 27.

Kwa mujibu wa tovuti ya Soccer Base, msimu uliopita mechi yake ya kwanza alicheza Septemba 13, 2015 dhidi ya Randers wakiwa ugenini, ambapo walifungwa 1-0. Na ya pili msimu huo, walikuwa nyumbani dhidi ya Hobro IK Novemba 29, 2015 walishinda mabao 2-0.

Msimu huu alicheza mechi ya kwanza Agosti 21, mwaka huu wakiwa nyumbani dhidi ya Midtjylland walitoka sare ya mabao 2-2 na ule wa pili alicheza Novemba 6, mwaka huu wakiwa ugenini dhidi ya FC Copenhagen, ambapo walifungwa 4-0 na siku hiyo alipewa kadi ya kwanza ya njano.

Simba-mauzo-ya-Emmanuel-Okwi-Bongosoka

Timu hiyo ina jumla ya wachezaji 45 lakini kati ya hao, kuna watano, ambao hawajawahi kucheza kabisa. Pia, wachezaji wanaocheza kikosi kikubwa wapo 27 kati ya hao 45 akiwemo yeye. Sio peke yake kucheza mechi mbili tu msimu huu, kuna wengine wamecheza mechi moja tu, na wengine hawajawahi kabisa.

Kutokana na kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha SonderjyskE, klabu yake ya zamani ya Simba imeonesha nia ya kumrejesha akikumbukwa kwa rekodi bora aliyoiweka misimu kadhaa iliyopita, ikiwemo kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa miaka kadhaa iliyopita.

Simba iko tayari kulipa dola za Marekani 120,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 240 kwa klabu hiyo ya Denmark kwa ajili ya kumrejesha Okwi. Inaelezwa kuwa iwapo kiasi hicho cha fedha kitalipwa mchezaji huyo atakuja kusaini mkataba wa mwaka mmoja kwa mshahara tu bila dau la kumsainisha.

Simba iliwahi pia, kumuuza Okwi Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2013 kwa dola 300,000 lakini hakudumu baada ya kuingia nao kwenye mgogoro na kurudi kwao kucheza SC Villa ya Uganda mwaka huo, na baadaye kujiunga na Yanga ambako alicheza muda mfupi na kurudi Simba.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com