Ligi kuu bila mdhamini mkuu , yote unayopaswa kujua…


Wakati ligi kuu ya Tanzania bara ikielekea katika Mzunguko wake wa pili , suala la kukosekana mdhamini mkuu wa ligi hiyo baada ya kampuni ya Vodacom Tanzania kumaliza mkataba wake limekuwa likisumbua vichwa vya wadau mbalimbali wa soka juu ya uwezo wa ligi kuu kufanikiwa bila mdhamini mkuu .

Lakini swali la kujiuliza ni je , inawezekana kwa TFF na Bodi ya ligi kufanikisha kuendesha ligi bila mdhamini mkuu ? Ikumbukwe Vodacom Tanzania walidhamini ligi kuu huku wakitoa kiasi cha Sh2.6 bilioni  kwa mwaka ambapo asilimia 57 ya fedha hizo zilienda kwa klabu kusaidia gharama za usafiri na mambo mengine.

Tukiendelelea kuchambua mgawanyo wa pesa hizo , asilimia 16 ya fedha za udhamini zilikuwa zikilipia gharama za waamuzi  huku asilimia 12.4 ya fedha za udhamini zikienda kwa waratibu ili kugharimia masuala ya kiutawala .

Kutokana na kukosekana kwa udhamini huu , ligi Kuu imeanza ikiwa na  wadhamini wadogo wawili tu. Wadhamini hao ni Azam Pay TV ambao wana haki za matangazo na benki rasmi ya Ligi Kuu (KCB Tanzania) ambao ni wadhamini wenza.

Kupitia udhamini huo kila klabu ya Ligi Kuu itapata kiasi cha Shi 177 milioni kwa msimu mzima ambapo Sh162 milioni ni fedha kutoka Azam Pay TV na Sh15 milioni kutoka Benki ya KCB Tanzania.

Pamoja na mapungufu haya ya udhamini , Tayari kampuni ya Vodacom Tanzania kupitia Mkuu wa Kitengo chake cha Masoko na Mawasiliano, Nandi Mwiyombella imeweka bayana kuwa wapo kwenye mazungumzo na TFF ya kuidhamini ligi kivingine , cha msingi ni kusubiria matunda ya mazungumzo haya yanayoendelea .

Ukiachana na Vodacom , taarifa rasmi kutoka kwa Mtendaji mkuu wa bodi ya Ligi, Boniface Wambura ziliweka wazi kuwa  ligi kuu itaendelea kama ilivyopangwa na watakuja kuwatangaza wadhamini wakati ikiwa inaendelea huku akibainisha wazi kuwa tayari wapo katika mazungumzo na makampuni mengi ambayo kati ya hayo mdhamini wa msimu uliopita Kampuni ya Mtandao ya Vodacom ni miongoni.

Kuhusu swala la vifaa kama jezi ambayo vilikua vikitolewa na mdhamini mkuu , Tayari TFF wameshakubaliana na  viongozi wa klabu zote za Ligi Kuu kutumia vifaa vyao kwanza mpaka mdhamini mkuu atapopatikana .

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com