Matokeo Simba VS Azam FC , Hakuna mbabe zatoka sare…..


Simba SC  leo imetoshana nguvu na Azam Fc kwa kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom uliopigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam. Magoli ya John Bocco na Ibrahim Ajibu yametosha  kuwafanya Simba na Azam FC kuweza kugawana pointi katika mchezo wa 10 wa ligi kuu ya vodacom.

Simba-VS-Azam Matokeo Bongosoka

Azam ndio walikuwa wa kwanza kuliona lango la Wekundu hao wa Msimbazi ambapo katika dakika ya kwanza tu ya mchezo, mshambuliaji John Bocco aliipatia timu yake bao la kwanza baada ya kutokea shambulizi la kushtukiza langoni mwa Simba.

Simba-VS-Azam-Matokeo Bongosoka 3

Baada ya bao hilo Simba walionyesha utulivu wa hali ya juu na kuendelea kucheza kama vile hawajafungwa bao huku viungo wake wa kati Said Ndemla, Justice Majabvi na Jonas Mkude wakitawala eneo hilo na kutengeneza nafasi kadhaa za mabao.

Katika dakika ya 25, kazi nzuri iliyofanywa na mlinzi wa kulia wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ilimaliziwa vema na Ibrahim Ajibu aliyeisawazishia Simba kwa shuti kali baada ya kuwapita walinzi watatu wa Azam.

Baada ya bao hilo Simba waliendelea kuliandama lango la Azam na kama si umahiri wa kipa wa Azam, Aishi Manula kuokoa hatari zote zilizoelekezwa langoni kwake na washambuliaji wa Simba, basi Simba ingeweza kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele.

Katika kipindi cha kwanza mwamuzi wa mchezo huo Erick Onoka kutoka Arusha alitoa kadi za njano kwa wachezaji wa pande zote ambao ni Ibrahim Ajibu wa Simba baada ya kuvua jezi wakati akishangilia bao alilofunga pamoja na Kipre Tchetche aliyejiangusha.

Ajibu aliifungia Simba bao la pili dakika ya 68 akitokea upande wa kushoto huku kipa wa Azam akiwa ametoka golini huku Bocco akiisawazishia timu yake bao la pili akiwa amepiga shuti iliyokwenda wavuni moja kwa moja dakika ya 74.

Simba-VS-Azam-Matokeo Bongosoka 2

Makocha wa timu hizo walifanya mabadiliko ambapo Dylan Kerr wa Simba aliwatoa Danny Lyanga, Abdi Banda na Emery Nimubona nafasi zao zilichukuliwa na Hamis Kiiza, Peter Mwalyanzi na Hassan Kessy wakati Stewart Hall wa Azam yeye aliwatoa Himid Mao, Salum Abubakar na Kipre Tchetche na kuwaingiza Michael Balou, Didier Kavumbangu na Yahaya Mudathir.

Mpaka dakika 90 zinamalizika timu hizo ziligawana pointi moja moja kwa  kutoka sare ya bao 2-2.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com