Mbwana Samatta atimiza ndoto yake , kutua bongo kesho…


Nahodha  wa timu ya Taifa (Taifa Stars) Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji amesema ndoto yake nyingine ya kucheza mashindano ya Ulaya imetimia.

Samatta alifunga bao la tano katika ushindi wa 5-1 dhidi ya Sporting Charleroi na kuifanya timu yake iweze kufuzu kushirikisho michuano ya Ulaya msimu ujao.

Straika huyo aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter juzi kuwa hiyo ni ndoto yake ya siku nyingi kucheza mashindano ya Ulaya na sasa anafurahi kuona amepata nafasi hiyo.

Mbwana-Samatta-Kolo-Toure-Bongosoka

“Hii ni ndoto ambayo sasa inatimia, namshukuru Mungu kwa jambo hili,” aliandika Samatta.

Aliongeza kuwa awali alipokuwa akicheza soka nchini, alikuwa na ndoto ya siku kucheza soka barani Ulaya na ndoto hiyo ilitimia mapema mwaka huu alipokamilisha uhamisho kutoka TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon na Simba zote za Dar es Salaam tayari ameichezea KRC Genk mechi 18 na amepachika wavuni mabao matano.

Nyota huyo anatarajiwa kuwasili nchini kesho ili kuiongoza Stars katika mechi ya Kundi G dhidi ya Misri kwa ajili ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Afrika (AFCON 2017).

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com