Ripoti ya kocha SIMBA yamuibua Mwamnyeto…


Baada ya ligi kusimama kwa siku 30 kutokana na tahadhari ya usambaaji wa virusi vya Corona, kocha wa klabu ya Simba Sven van De Broek, alitajwa kuwasilisha ripoti ya utendaji kazi kwa viongozi wa klabu hiyo ambayo ilikuwa na mapendekezo mbalimbali.

Ripoti yenyewe…

Baadhi ya mambo, yaliyotajwa kuainishwa katika ripoti hiyo, ni kama yafuatayo kama alivyoripotiwa kunukuliwa CEO wa Simba, Senzo Mbatha:

“Katika hili la usajili tumeanza tayari skauti katika maeneo mengi hapa Afrika, ili kupata wachezaji bora na imara pengine tutafanya usajili mzuri kuliko misimu yote, kwani kuna vigezo vingi kulingana na mahitaji yetu. Hatutasajili kwa mihemko,”

 “…tumeanza kuangalia wachezaji katika ligi ya ndani ambapo tunaweza kusajili hata wawili na maeneo mengine Afrika katika nchi ambazo zimeendelea kisoka…,”

Mwamnyeto chaguo la kwanza…

Inasemekana katika mapendekezo ya nafasi za kuimarishwa ndani ya Simba, Kocha Sven Van De Broek anahitaji beki wa kati, mwenye umri mdogo ili kuimarisha safu ya Ulinzi ya timu hiyo.

Katika juhudi za kutimiza mapendekezo hayo, imeripotiwa kwamba tayari viongozi wa Simba, wameanza mapema harakati za kumtwaa beki kisiki na nahodha wa Coastal Union, Bakari Nondo Mwamnyeto ambaye amekuwa katika kiwango kizuri siku za karibuni ndani ya klabu na timu ya taifa, Taifa Stars.

Kutengewa mamilioni na gari…

Moja ya chanzo cha uhakika, kimeripoti kuwa Mwamnyeto ametengewa shilingi milioni 85 pamoja na gari aina ya Toyota Crown, ili aweze kukubali ofa hiyo na kuwatumikia wekundu hao wa Msimbazi kuanzia msimu ujao.

Licha ya kuwa timu iliyoruhusu magoli machache zaidi katika ligi msimu huu, bado Simba inatajwa kuwa na upungufu katika eneo la ulinzi, hali inayotajwa kuwa ni kutokana na miili ya wachezaji wa eneo hilo kushindwa kuhimili kasi ya mchezo.

“Kutokana na uwezo wake na umri wake, Mwamnyeto anaonekana kuwa ingizo sahihi kukidhi vigezo vya kocha, hali inayowafanya viongozi kuweka nguvu kubwa katika kumpata,” kilieleza chanzo hicho.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com