Simba kibaruani leo dhidi ya Kagera Sugar…


Klabu ya wekundu wa msimbazi , Simba leo wanashuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu ili kuzidi kujikita kileleni wakati watakapocheza dhidi ya Kagera Sugar.

Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Uhuru huku Stand United wanaoshika nafasi ya pili wakiwa wenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.

Hizi ndizo timu zinazokimbizana kwa pointi hivyo, macho yote yataelekea kwao. Simba ndio vinara wa ligi kwa pointi 20 katika michezo nane waliyocheza, wakijivunia kutopoteza mchezo hata mmoja, tangu kuanza kwa msimu huu.

Timu hiyo ya Msimbazi huenda ikaendeleza ushindi baada ya kutoka kuifunga Mbeya City mabao 2-0 ugenini, kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya Jumatano.

muzamir-simba-uwanja-wa-uhuru

Lakini pia, Kagera Sugar haiko katika kiwango kibaya msimu huu, kwani inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 15 katika michezo tisa iliyocheza.

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime alisema anataka kuvuruga sherehe za Simba kwa kuhakikisha wanainyamazisha. Licha ya tambo za wenyeji, itakumbukwa msimu uliopita Simba ikiwa katika kiwango kibaya iliifunga Kagera Sugar nyumbani na ugenini, ambapo kwenye Uwanja wa Taifa ilishinda 3-1 na ugenini bao 1-0.

Mchezo huo huenda ukawa mgumu, kwani Simba itataka kushinda ili kuendelea kubaki kileleni, na Kagera inataka ushindi iendelee kuwa katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo yenye jumla ya timu 16.

Aidha, kama ilivyo kwa Simba hata Stand United imekuwa ni bora ikijivunia kutopoteza mchezo hata mmoja. Leo itaikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa CCM, Kambarage Shinyanga. Timu hiyo msimu huu imekuja kivingine baada ya kuwapiga vigogo wawili kwenye uwanja huo, yaani Yanga na Azam zote zikifungwa bao 1-0 kila moja.

Hii ndio timu inayoifukuzia Simba kwa pointi 19, hivyo ni lazima itapambana kuendelea kulinda nafasi yake. Inakutana na timu ambayo ambayo iko katika kiwango cha kawaida ikiwa na pointi tisa katika michezo tisa.

Pia, Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya tano kwa pointi 14 nayo itaendelea kusaka ushindi kwenye Uwanja wa Manungu dhidi ya Tanzania Prisons ambayo nayo, haiko vizuri sana msimu huu, ukilinganisha na msimu uliopita. Tanzania Prisons inashika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 10 katika michezo nane iliyocheza.

Timu zote mbili zinahitaji ushindi kwani atakayepoteza atakuwa kwenye uwezekano wa kushuka kutoka nafasi moja hadi nyingine. JKT Ruvu na Mwadui zitakutana zote zikiwa haziko katika nafasi nzuri.

Mwadui ina pointi nane katika michezo nane ikishika nafasi ya tatu kutoka mwisho, na JKT Ruvu inashika nafasi ya nne kutoka mwisho ikiwa na pointi nane sawa na Mwadui.

Kila mmoja anahitaji ushindi kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja. Vile vile, Majimaji ambayo inashika mkia itakuwa ugenini dhidi ya Toto African kwenye uwanja wa CCM, Kirumba, Mwanza.

Timu hiyo ina pointi tatu ikishika nafasi ya mwisho, ikifuatiwa na Toto inayoshika nafasi ya pili kutoka mwisho ikiwa na pointi nane, wote wakiwa wamecheza michezo tisa.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com