Simba , Umefika wakati kusahau yaliyotokea…


bila shaka ilikuwa ni wiki yenye pilikapilika nyingi katika tasnia ya mpira wa miguu Tanzania, mashabiki na wapenzi wa simba sc hawataisau wiki hii kwa kuwa ilikuwa yenye machungu mengi kwa upande wao, si nia yangu kukumbusha machungu ila hakuna njia ya kutatua tatizo isipokuwa kukabiliana nalo, mbio za sakafuni huishia ukingoni, hakuna marefu yakakosa ncha pia barabara ndefu haikosi kona. Dhahiri maamuzi yaliyofanywa na kamati ya sheria na hadhi za wachezaji kupelekea singano kujiunga na azam fc yatakuwa yamewaumiza wapenzi wengi wa simba sc, si wakati wa kumfikiria asiye kufikiria, ni wakati sasa wa kujenga timu yenye msingi imara kupitia vijana waliopo. Yupo. Peter Mwalianzi na Simon Sserunkuma ambao wanauwezo wa kucheza alipokuwa akicheza singano.

Ramadhan-Singano-emmanuel-Okwi-bongosoka-web

 

Wakati ya Singano yakiwa hivyo imetoka taarifa ya usajili wa Okwi nchini Denmark, hapa furaha na huzuni vimekutana mioyoni mwa wanamsimbazi, wapo watakaofurahishwa na jambo hilo kutokea lakini wapo watakao huzunishwa nalo. Maswali mengi yanazunguka vichwani mwa wanamsimbazi lakini hili halitakuwa na majibu kwao. Nani mtu sahihi kuziba nafasi ya Okwi?, kumbuka kabla Okwi hajafuzu majaribio yake alisajiliwa Mganda Hamis Kiiza ‘Diego’, hana vitu vingi kama okwi lakini linapokuja suala la kufumania nyavu hapa utamkuta kwenye kibendera cha kona uwanja ukilipuka kwa shangwe, analijua sana goli huyu jamaa, sijui kwanini yanga walimuacha labda hakuendana na mfumo wao. Linapokuja suala la usajili wa wachezaji wa kimataifa ninawaamini sana simba sc kuliko timu yeyote hapa Tanzania. Usajili wa Juuko Murshid una mchango mkubwa sana kikosini hapo, usajili wa Amisi Tambwe kutokea Vital’O ya Burundi ulikuwa na impact kubwa msimbazi ingawa ilimaliza ligi katika nafasi ya nne. Sisemi hawasajili magarasa ila wanajitahidi kwa kiasi fulani, wapo magarasa kama Abel Dhaira mlinda mlango huyu, Komanbil Keita mlinzi wa kati, Mussa Mude japokuwa hakuwa garasa sana lakini alishindwa kuisaidia timu ipasavyo.

Emmanuel-Okwi-simba

Kwa upande mwingine bado dirisha la usajili halijafungwa hivyo uwezekano wa kumtafuta okwi mwingine upo, inawezekana ikawa furaha kwa upande wa pili wengi hawatamsahau kwa goli lake aliloifunga yanga uwanja wa taifa baada ya kuwatoka walinzi wa yanga na kuachia mkwaju mkali uliomshinda mlinda mlango wa yanga, si hivyo tu mchango wake katika timu yake ulikuwa ni mkubwa. Haipingiki ameacha pengo ambalo kuzibika inahitajika akili, wanasimba sahauni yote yaliyopita anzeni mikakati ya kujenga timu itakayoleta upinzani katika ligi ijayo ambayo itakuwa na timu 16, sare sita mfululizo mwanzoni mwa ufunguzi wa ligi iliyomalizika liliwaumiza sana lakini sasa yote hayo ni historia, historia mpya ya simba sc msimu ujao inategemea maandalizi ya leo, hata iweje singano na okwi hawatarejea kwa sasa cha msingi ni kuwasahau ingawa si rahisi kutokea…msambaa mmoja havunji soko ulipoangukia inuka uanzie hapo kwenda mbele.

->Makala hii imeandikwa na Halidi Abdulrahman.

 

 

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com