Simba VS Mbao FC hapatoshi leo fainali ya kombe la shirikisho…


Klabu za Simba SC na Mbao FC leo zitakua na mtiahani mzito pale zitakapomenyana kwenye fainali ya  kuwania ubingwa wa kombe la shirikisho na nafasi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika  kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Timu zote mbili leo zinacheza fainali kwa mara ya kwanza, Simba iliifunga Azam FC bao 1-0 katika mchezo wa hatua ya nusu fainali na Mbao FC pia walipata matokeo ya aina hiyo kwa kuwavua ubingwa Yanga katika mchezo uliofanyika jijini Mwanza.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alisema kuwa wanatarajia kukutana na changamoto na ushindani katika dakika zote 90 za mchezo huo.

Omog alisema kila upande unahitaji nafasi hiyo moja iliyobakia ili kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani na wataingia uwanjani kuwakabili wapinzani wao kwa tahadhari.

“Ni mechi ngumu, kikubwa ni wachezaji kutokuwa na presha ya nje ya uwanja, ni mchezo muhimu sana kwetu kwa sababu utatupa matokeo yatakayofunga ripoti ya msimu wa 2016/17, tuna matumaini ya kupata matokeo mazuri,” alisema Omog.

Aliongeza kuwa ushindi katika mechi hii ya fainali utarejesha furaha ya wanachama na mashabiki wa Simba ambao kiu kubwa waliyonayo ni kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani.

Naye Kocha Mkuu wa Mbao FC, Etienne Ndayiragiye, alisema kuwa amewaandaa vizuri wachezaji wake kwa ajili ya kuweka rekodi mpya kwenye mchezo wa soka hapa nchini.

“Sina maneno mengi, Simba ni timu kubwa lakini timu yangu pia imejipanga, tunajua ushindi utatufanya tupate wadhamini wa kusaidia klabu yetu, ni mchezo utakaokuwa na ushindani,” alisema kocha huyo.

Mbali na kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, bingwa wa kombe hilo atazawadiwa kitita cha Sh. milioni 50.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com