Taifa stars fanyeni kweli mechi ya leo…


TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo inashuka dimbani kucheza na wenzao wa Uganda, The Cranes, katika mchezo wa marudiano wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan). Mchezo huo ni muhimu kwa Taifa Stars baada ya kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar, hivyo timu hiyo inahitaji angalau ushindi wa kuanzia mabao 4-0 ili isonge mbele. Stars wakati inafungwa na Uganda katika mchezo wa kwanza, ilikuwa chini ya Mholanzi Mart Nooij lakini sasa iko chini ya kocha mzawa, Charles Mkwasa na jopo lake la benchi la ufundi. Hakuna asiyejua kuwa Taifa Stars ina kibarua kizito cha kuiondoa The Cranes, lakini matarajio ya wengi ni kuwa, timu hiyo itashinda bila kujali idadi ya mabao baada ya wadau wa soka kuchoshwa na vipigo vya timu hiyo. Kipindi cha Nooij tumeshuhudia Taifa Stars kucheza mechi kibao zikiwemo za kirafiki na zile za kimashindano, lakini aliishia kufungwa nyingi ya michezo iliyocheza timu hiyo. Inasikitisha kuona timu hiyo ilicheza mechi 16 na ilifungwa mechi saba, sare sita na kushinda tatu tu chini ya Mholanzi huyo aliyetimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Mkwasa. Tena cha kusikitisha zaidi katika mechi hizo za kufungwa, mechi tano ilifungwa mfululizo na kuzidisha hasira kwa wapenzi wa soka hapa nchini.

Mazoezi-ya-Taifa-Stars-3

Mara kadhaa timu hiyo imeshindwa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), ambazo kwa mara ya mwisho Tanzania ilifuzu mwaka 1980 zilipofanyikia Lagos, Nigeria huku zile za Chan kwa mara mwisho tulifuzu mwaka 2009 nchini Ivory Coast na timu ikiwa chini ya Mbrazili Marcio Maximo. Baada ya Mkwasa na benchi lake la ufundi kuinoa kwa muda mfupi timu hiyo, ni matarajio kuwa wachezaji kwa kutumia mbinu walizofundishwa na makocha, wataitoa kimasomaso Tanzania kwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo. Watanzania wanataka Taifa Stars ishinde hata kama itashindwa kusonga mbele kwani wamechoka kuona timu yao ikifanya vibaya kila kukicha na kuwa sawa na kichwa cha mwendawazimu, ambacho watu hujifunzia kunyoa. Wakati umefika sasa kwa wachezaji wa Taifa Stars kukataa kuwa vibonde na kufungwa na kila timu wanayokutana nayo katika mashindano mbalimbali, na badala yake kupigana kiume na kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

Kikosi-cha-Taifa-Stars

Wapenzi nao wanatakiwa kuwa na subira na kuwapa muda zaidi akina Mkwasa ili waweze kuiunda vizuri timu hiyo, kwani wameichukua wakati tayari imeanza mashindano, hivyo watachukua muda kuiweka sawa. Mchezo wa leo ni wa kurejesha heshima baada ya timu hiyo kufanya vibaya kwa muda mrefu chini ya Nooij, huku kocha huyo akigoma kujiuzulu mwenyewe hadi pale Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipoamua kumtupia virago. Watanzania wako nyuma ya wachezaji, viongozi na benchi lote la ufundi la Taifa Stars wakiomba dua ili kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri nchini Uganda, hivyo msiwaangushe.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com