TFF yaingilia swala la Hassan Kessy , Yanga yaomba mechi yao ipelekwe mbele..


SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) limesema litaingilia kati kama klabu ya Simba itachelewa kujibu maombi ya Yanga ya kumtumia beki Hassan Kessy kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF-CC).

Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) liliizuia klabu ya Yanga kumtumia beki Hassan Kessy kwenye mchezo dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria mpaka pale klabu yake ya zamani Simba iandike barua ya kuiruhusu Yanga ambayo itaituma kwenye shirikisho hilo kama uthibitisho ya kuwa hana mkataba na klabu yake hiyo ya zamani.

Yanga iliiandikia barua klabu ya Simba juzi na nakala ya barua hiyo kuiwasilisha TFF wakiwataka mahasimu wao hao kutoa ruhusa kwa beki Hassan Kessy ambaye mkataba wake na klabu yake hiyo ya zamani unafikia kikomo Juni 30 kuichezea timu hiyo kwenye kombe hilo.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alithibitisha kupokea nakala ya barua hiyo ya Yanga kwenda kwa mahasimu wao Simba juzi na kusema wanafuatilia kama watajibiwa kwa wakati.

Hassan-Kessy-Yanga-Simba

“Tusingeweza kuingilia kati suala hili mpaka Yanga wenyewe waiandikie Simba kuomba ruhusa yao na kama Simba watachelewa kuwajibu Yanga, sisi tutaingilia kati kwa kuwapa taarifa CAF kuwa Kessy hana mkataba na Simba na aruhusiwe kuichezea Yanga,” alisema Lucas.

Alisema kwamba kwa kawaida mchezaji akibakiza muda fulani wa mkataba wake anaruhusiwa kujiunga na timu yoyote na ndivyo ilivyo kwa Kessy, ingawa Simba wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa Yanga kama taratibu za CAF zinavyojieleza.

Katika hatua nyingine, TFF imesema kuwa imepokea maombi ya Yanga ya kutaka shirikisho hilo kuiandikia CAF wakitaka mchezo wao wa Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika(CAF-CC) dhidi ya TP Mazembe uchezwe Juni 29 badala ya Juni 28.

“Yanga walipewa nafasi ya kuchagua tarehe tatu za mchezo huo kufanyika ambapo ni tarehe 28, 29 na 30 na CAF na walitakiwa wachague moja ya tarehe hizo na kuthibitisha CAF, lakini hawakufanya hivyo na CAF kuamua mechi hiyo ichezwe tarehe 28 saa 10:00 jioni. “Sasa wamekuja wakitaka tuwasaidie kuwaombea CAF ili mchezo wao uchezwe Juni 29 saa 7:30 usiku kwa hoja ya kutoa nafasi kwa baadhi ya mashabiki wao ambao baadhi yao ni waumini wa dini ya Kiislamu kuweza kushuhudia mechi hiyo na tayari tumeshawaandikia CAF na tunasubiri majibu yao,” alisema Lucas.

Aidha, Lucas aliishutumu klabu ya Yanga kwa kushindwa kutuma mtu kuhudhuria semina maalumu iliyoandaliwa na CAF kwa ajili ya mashindano hayo ambayo kwenye semina hiyo wangepata elimu juu ya mambo mbalimbali kuhusu ushiriki wao.

“Inashangaza sana CAF waliwatumia Yanga barua ya mwaliko mapema sana na mwenyekiti wao Yusuph Manji alithibitisha kuipata barua hiyo, lakini wakaipuuza. Wangetuma mtu kwenye semina ile ambayo CAF walikuwa wanagharamia kila kitu wangepata elimu kubwa ya ushiriki wao kwenye mashindano yao.

“Madhara ya kutoshiriki semina hiyo ndio kama hayo ya kontena lao la vifaa kama vile viatu, vifaa vya mazoezi, jezi za mechi ambazo zingetoa nafasi ya wao kuweka nembo ndogo ya mdhamini wao (Kilimanjaro) mabegani. Hawakuwa na jezi hizo kwenye mchezo wa kwanza na walilazimika kununua jezi nyingine,” alisema Lucas.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com