Usajili 9 ghali zaidi ligi kuu Tanzania bara msimu huu


Wakati ligi kuu inakaribia kuanza hapo September 12 , bongosoka tumeona ni vizuri kuchambua  baadhi ya wachezaji waliogharimu timu zao kuvunja benki ili kuhakikisha zinatwaa taji la ligi kuu ya Vodacom msimu wa 2015/2016 . Huku tayari TFF ikipitisha idadi ya usajili wa wachezaji wa kigeni isizidi  7 , tayari inaonekana wazi kwamba wachezaji wengi ghali ni wa kimataifa na ndio wanaokula mishahara minono ukilinganisha na wachezaji wa ndani. Yanga pia ndiyo timu yenye kikosi ghali zaidi nchini na wachezaji wake ndiyo wanaolipwa ghali zaidi ukiachilia mbali wale wa Azam ambayo inamilikiwa na Bilionea, Said Salim Bakhresa.Hii ni 9 bora  ya usajili wa gharama  ambao uliwekwa wazi msimu huu unaoanza :-

Usajli-Ghali-ligi-kuu-Tanzania-copyright-bongosoka-com 2

9. Mussa Hassan Mgosi (Mtibwa Sugar   kwenda Simba    | milioni 8 za Tanzania )

SIMBA SC ilifanikiwa tena  kumsajili mshambuiaji wake wa zamani, Mussa Hassan Mgosi ,  baada ya takriban misimu miwili mizuri akiwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro.

 

8. Peter Mwalyanzi  (Mbeya City   kwenda Simba    | milioni 15 za Tanzania )

timu  ya Simba nayo ilifanikiwa  kumnyakua kiungo wa Mbeya City Peter Mwalyanzi kwa mkataba wa miaka miwili ambapo walitoa milioni 15 kwa uhamisho wake.

 

7. Gideon Brown   (Ndanda FC  kwenda  Mbeya City  | milioni 15 za Tanzania )

Mshambuliaji  mpya wa Mbeya City , Gideon Brown amesajiliwa na timu hiyo hivi karibuni akitokea Ndanda FC, ametua kwenye timu hiyo akibebeshwa najukumu mazito na kocha Juma Mwambusi  huku akiwa amebeba matumaini ya maelfu ya mashabiki na viongozi wa timu hiyo kuwa anaweza kulipa fadhila na kurudisha garama za pesa zilizotumika kumsajili.

 

6. Malimu Busungu(Mgambo JKT  kwenda Yanga | milioni 25 za Tanzania )

Yanga ilizidi kuimarisha safu yake ya Ushambuliaji baada ya kukamilisha sahihi ya aliyekua mshambuliaji  hatari wa Mgambo JKT , Malimi Busungu kwa ada ya uamisho ya milioni 25. Busungu alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga kuanzia  msimu utakaoanza hivi karibuni.

 

5. Hamisi Kiiza (Mchezaji Huru  kwenda Simba  | milioni 35 za Tanzania )

Kiiza amesajiliwa na Simba akiwa mchezaji huru baada ya kutemwa na Yanga msimu uliopita akidaiwa ameshuka kiwango lakini Simba wanaamini bado mchezaji huyo anauwezo wakuwasaidia kufanya vizuri na kuamua kumsajili kwa kumpa misimu miwili huku akiigarimu timu hiyo milioni 35.

 

4. Deus Kaseke (Mbeya City  kwenda Yanga | milioni 35 za Tanzania )

Deus Kaseke  alijiunga na Yanga baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili ambapo alitoa kali ya mwaka mara baada ya kutambulishwa tu, ambapo kiungo huyo alitaka mambo mawili. Kwanza,  apewe jezi namba nne ambayo Yanga walimpa na  pili alitaka  kocha amchezeshe winga wa kushoto, ili aweze kuifanyia makubwa klabu hiyo.

 

3. Ramadhan Singano (Mchezaji Huru  kwenda Azam  | milioni 50 za Tanzania )

SIKU mbili baada ya kupewa haki ya kuwa mchezaji huru, winga Ramadhan Yahya Singano ‘Messi’ alifanikiwa kusaini Mkataba wa miaka miwili kujiunga na Azam FC  kwa usajili wa milioni 50 ambapo atakuwa akilipwa milioni 2 kwa mwezi.

 

2. Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya ya Qatar kwenda Simba  | Dola 25,000 / milioni 50 za Tanzania )

Simba ya Dar es Salaam  ilifanikiwa kumrejesha nyumbani kiungo wake Mwinyi Kazimoto kwa dau la Dola za Kimarekani  25 elfu sawa na milioni 50 za kitanzania. Mshahara wa Kazimoto kwa mwezi ni  Sh2 milioni ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili. Kwa maana hiyo, Kazimoto ataikomba Simba jumla ya Sh 98 milioni kwa miaka miwili ambapo fedha ya usajili ni Sh 50 milioni wakati mshahara kwa miaka miwili ni Sh 48 milioni.

 

1. Donald Ngoma  (FC Platinum ya Zimbabwe  kwenda Yanga  | Dola 50,000 / milioni 100  za Tanzania )

Aliyekua mshambuliaji tegemeo wa FC Platinum, Donald Ngoma alitua kwa vigogo wa Tanzania, Yanga SC  kwa usajili wa Dola za kimarekani 50,000. Ngoma, ambaye mkataba wake unamalizika Platinum mwishoni mwa msimu ujao, aliivutia Yanga wakati timu hizo zilipokutana katika mchezo wa 32 Bora Kombe la Shirikisho Afrika na ndipo walipoamua kumsajili huku tayari akiwa ashaonesha maufundi yake kwenye michuano ya Kagame.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com