Usiyatarajie ya Leicester City kwenye Ligi ya Tanzania


WENGI wameshangazwa na ilikotokea klabu ya Leicester City na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu. Kutokana yale yaliyofanywa na Leicester basi wengi wamekuwa na mawazo kwamba huenda hilo pia linaweza kutokea siku moja kwenye ligi yetu ya soka Tanzania Bara.

Mawazo haya kwamba ya Leicester yanaweza kutokea Tanzania naona yanabaki kuwa mawazo tu, kwa maana hayatatokea kabisa kwenye soka letu la Tanzania na huo ndio ukweli.

leicester-city--Bongosoka

Lazima tuambizane ukweli ingawa wengine hawautaki na kuna sababu nyingi sana na za msingi mno kuona kwamba mambo hayo hayawezekani kutokea.

Baada ya mabingwa hao wapya wa England kutwaa taji kuna maneno mengi yanasemwa, eti hapa Tanzania pia inawezekana lakini kila nikilitazama soka la nchi yetu na mfumo wake naona wazi kwamba suala hilo haliwezekaniki.

Niapozungumzia mfumo wa soka letu bila shaka mashabiki na wapenzi wa mpira wanaelewa ninachomaanisha, kwani watakuwa mashahidi wa kile kinachoendelea kwenye ligi yetu ikiwemo hali ya figisu figisu nyingi kupita uhalisia.

Hakuna ubingwa wa kweli kwenye nchi hii ingawa wenyewe hatutaki kusema kweli, ila nafsi zinatusuta na huo ndio ukweli wenyewe. Ligi yetu ni ya hovyo mno haistahili hata kuitwa ligi kuanzia kwa hao wanaosimamia hadi wachezaji wenyewe ambao nao wanajua kuwa hali si nzuri.

Kuna timu kwenye Ligi ya Tanzania zinashuka daraja ila hazistahili kushuka kwa sababu tu wameshindwa kwenye fitina na mizengwe mingi inayoendelea kwenye soka lenyewe.

Ligi yetu ina madudu mengi ambayo hayastahili kuwemo kwenye soka, ila yanalelewa tu ilimradi tu yanawabeba watu fulani na yanafanywa kwa maslahi ya watu fulani na si kwa ajili ya Soka la Tanzania.
Ninarudia tena ya Leicester City hayawezi kutokea kwenye ligi yetu kwani kwenye ligi yetu kuna masuala ya ‘miamala ya pesa’ au ya ujumbe wa kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na Whatsapp.
Haiwezekani tusiumize vichwa maana kuna watu wameng’ang’ania ukweli ila acha niwaambie ukweli. Nafahamu wengine wanayo kumbukumbu ya Mtibwa Sugar kuchukua ubingwa mara mbili mfululizo na pengine Azam kuleta changamoto mpya.

Nakubali lakini labda tuizungumzie Azam si timu nyingine ambazo zimeshajihakikishia kuwa ni washiriki wa kudumu wa ligi na pengine wafanyabiashara kwenye mechi muhimu inapotokea.

Kuna uhovyo ambao haustahili kufumbiwa macho lakini sisi japo hatujafumba macho, tumeuacha na unaendelea kwenye ligi yetu kana kwamba hatuoni vile kwa sababu tu kuna watu wenye misuli na uhovyo huo kwenye kuliongoza soka letu.

Kuna msemo mmoja wa Kichina unasema, kama wewe hutaki kuna wenzio wanaotaka na ndicho kinachoendelea kwenye Ligi ya Tanzania, kuna wachache wanayataka hayo maovu na ndio wameshika mpini basi wanafanya wanavyotaka na wanaendelea kuiharibu ligi yetu.

Leicester City ilikuwa bingwa wa England kwa sababu waamuzi wilikuwa hawapewi ‘maagizo’ kama inavyofanyika kwenye ligi ya hapa kwetu. Ingawa hamtaki tuseme ila sasa tunasema kwa sababu wenyewe mmeyataka na tumechoka na madudu yenu.

leicester-city--Bongosoka-2

Leicester City imechukua ubingwa kwa sababu hakuna usajili wa wachezaji wa ‘ten percent’ kama unavyofanyika kwenye soka la Bongo. Hata kwenye ligi kuna baadhi ya timu kila kiongozi ana mchezaji wake na huyo mchezaji anacheza kulingana na maelekezo ya huyo kiongozi na si kocha.

Leicester City imetwaa ubingwa kwa sababu kwenye EPL hakuna magoli ya kununua, nadhani wenyewe mnajua inavyofanyika kwenye soka letu ambalo limetiwa mfukoni kama noti.

Leicester City imetwaa ubingwa kwa sababu kwa wenzetu hakuna siasa ya soka ya kuzitukuza baadhi ya timu na ndio maana ninasema hayo hayatokei kwenye ligi yetu hadi tuyaache makandokando yote.

Ya Leicester City hayawezekani kwenye ligi yetu ambayo timu zake hazina mfumo mzuri wa kukuza wachezaji na longo longo lukuki.

Lazima tuseme kweli madudu mengi ya kwenye ligi yetu yanajulikana ila hatutaki tu kusema ukweli na pengine hata ukweli ukisemwa hakuna anayejali na ndiyo maana madudu hayo yanazidi kutumaliza na kuliangamiza soka letu.

Ifike wakati tuwe wa kweli na tuamini kwenye ukweli ili tuweze kufika walikofika wenzetu na hapo ndipo yanaweza kutokea haya ya Leicester City.

Makala hii imeandikwa na MO VAN DER MHANDO (0676121979)

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Bonyeza hapa kupata offer kabampe. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com