Vichekesho sita vinavyoyumbisha soka la bongo


Kama wewe ni mfuatiliaji wa mpira wa miguu kimataifa basi utakua ni miongoni mwa watu wanaojiuliza hivi kwanini ukiangalia mechi ya nje ina utofauti mkubwa sana na inayochezwa kwenye ligi ya nyumbani au timu ya taifa . Hivi tokea mashindano ya ligi kuu yalipoanzishwa  mwaka 1965  huku  ikishirikisha klabu za Dar es Salaam pekee ,  ni nini tumeweza kujifunza na kukiendeleza tokea ligi hiyo ianzishwe ? Wakati ligi inaanzishwa bado hatukuwa wanachama wa FIFA na miaka kadhaa kupita  Yanga ilifungua historia ya ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye michuano ya Afrika mwaka 1969, baada ya kutwaa ubingwa wa nchi kwa mara ya kwanza mwaka 1968, kabla ya kuutetea mara nne mfululizo, katika miaka ya 1969, 1970, 1971 na 1972. Baada ya hapo, Sunderland ikiwa tayari imebadili jina na kuitwa Simba kurejesha taji lake mwaka 1973 , lakini miaka hii yote klabu hizi kongwe zinashindwaje  kua na maendeleo kama uwanja wa kisasa ? Hivi unajua Taifa Stars imefuzu kushiriki mashindano ya mataifa ya Afrika mara moja tu ? Katika kikosi kilichokua na watu kama aliyekuwa rais wa TFF , Leodgar Tenga , ambapo  ilikua ni agosti 26,1979 Taifa Stars ilipokua  ikihitaji sare ya aina yoyote dhidi ya Zambia ili ifuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki mwaka 1968.  Bao  la Peter Tino  lilinyamazisha umati wa mashabiki wa Zambia waliokuwapo uwanjani kwani liliiwezesha Taifa Stars kufuzu kushiriki  kwa mara ya Fainali za Mataifa ya mwaka 1980 zilizofanyika Lagos, Nigeria ambapo ni miaka 35 imepita bado watanzania wana kiu ya kuona timu yao ikirudia historia hii isiyoweza kusahaulika. Lakini swali la kujiuliza ni je, tatizo ni nini ? hizi ni baadhi ya sababu ambazo naweza kuziita “Vichekesho” , zinazoyumbisha soka la bongo :-

Taifa--Stars-kocha-yanga-simba-azam-bongosoka-malinzi-tff

1 . Madudu ndani ya TFF

Kuna msemo usemao , ukitaka kutatua tatizo inabidi kwanza utafute chanzo au mzizi wake upo wape kisha uukate. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekua likilalamikiwa kila siku juu ya uozo uliopo katika maamuzi yake na jinsi kinavyoendesha soka la bongo. hivi juzijuzi Rais kikwete alipokua anavunja bunge alikata mzizi wa fitina baada ya kusema yeye sio sababu timu ya taifa inafanya vibaya ambapo alisema katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake aliahidi  serikali itamlipa kocha na imefanya hivyo . Kwa kusema hayo ni nani mwenye maamuzi ya kutafuta Kocha mwenye uzoefu ambaye anaweza kubadilisha mtazamo wa wapenzi wa soka kama si TFF? kichekesh kingine kutoka kwa TFF ni mfumo mbovu wa ligi unaolalamikiwa kila siku , Nakumbuka msimu wa ligi 2014/2015 mechi ya ufunguzi Mtibwa sugar walikifunga kikosi cha Yanga mabao 2 bila majibu , kikosi ambacho   kilikuwa na wachezaji wanne wa kimataifa na sita wa timu ya Taifa ambao ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mrisho Ngassa na Saimon Msuva pamoja na wachezaji wanne wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite Jr, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ , Haruna Niyonzima na Hamis Kiiza huku  Mtibwa Sugar ambayo haina hata mchezaji mmoja wa timu ya Taifa wala wa kimataifa. Miaka ya 1980 timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliifunga timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars mabao 5-0. Kikosi hicho cha Stars kilikuwa na wachezaji wawili tu kutoka Simba na wawili kutoka Yanga tofauti na ilivyo sasa hivi.  Ligi kuu Haizalishi wachezaji wa kutosha, haina ushindani na kwa maana hiyo ni ndoto kuwa na Taifa Stars bora.  Sitaki kuongelea madudu ya tiketi za elektroniki (ETS) , mikataba , usajili , kuvujwa kwa kanuni za ligi na mengine kibao maana nitawachosha.

 

2.  Uongozi mbaya ndani ya vilabu

Ni juzijuzi tu hapa tumesikia story mbili kubwa kutoka uongozi wa vilabu vikongwe  ambapo Uongozi wa Simba ukituhumiwa kumuongezea mkataba na kukeuka vipengele vya kimkataba huku nao Yanga wakilalamikiwa na timu inayoshiriki ligi daraja la kwanza kwa kumuiba mchezaji wao hadi pale walipoipoza timu hiyo kwa milioni 7, hivi ushawahi kusikia mambo kama haya kwenye vilabu vya nje ? eti mchezaji anadai mkataba wake umeisha huku uongozi ukisema bado mwaka mmoja, hivi si vichekesho jamani ? kwanini soka la bongo lisihamasishe vilabu vikafuata kanuni na taratibu za uendeshaji vilabu za kimataifa ? Haya, tetesi nyingine tumesikia Azam wanataka kupeleka kikosi cha pili michuano ya Kagame….nani anakumbuka mwaka 2014 , Yanga ilitaka kupeleka kikosi cha wachezaji inaowataka huku waandaaji Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) likitaka kikosi cha kwanza. Malumbano yalikuwa mengi na Cecafa ilikataa kupokea kikosi cha wachezaji vijana na wale wasio na nafasi kikosi cha kwanza waliotaka kuepelekwa na kocha msaidizi badala ya Maximo ambaye alipanga kwenda na timu kambini Zanzibar. Hivi kama si vichekesho ni nini sasa?

3. Kukosekana ufanisi uwanjani

Kama na wewe utakua makini sana katika kuangalia na kufananisha aina za uchezaji unapoangalia mechi ya Manchester na Yanga basi utakua umeshagundua jinsi ambavyo wachezaji wanajipanga uwanjani. Ukiangalia mechi ya Manchester hauna haja ya kujiuliza “formation” wanayocheza kwani jinsi wanavyojipanga uwanjani basi wewe mwenyewe utafurahi, sasa angalia mpira wa  bongo, wachezaji hawachezi kwa formation bali wanakimbiza mpira, hauwezi ukaona ufanisi uwanjani , basi za bila kuangalia , 1 2 hivi zinakosekana sana yani unaangalia mpira ushajua pasi anapewa mtu yule alafu itaenda kwa yule. Mpira ni zaidi ya uwanja , wachezaji inabidi wapewe mafunzo ya kutosha juu ya mbinu za uwanjani na sio tu za kucheza hata kisaikolojia.

4. uozo wa marefa

Kama wewe ni refa hapa Tanzania basi nakusihi kabla ya kuanza urefa uende jeshini kupata mafunzo ya kijeshi kukabiliana na wachezaji na mashabiki wenye hasira kali pale tu utakapotoa maamuzi ambayo hawakubaliani nayo . hiki ni kitu cha kushangaza sana kwenye mpira wa Tanzania, ni kwanini marefa hawaheshimiki na wanapigwa kila siku ? hii kituinaua sana mpira wetu bila tu sisi kujua.  Kanuni ya 37(5) ya Ligi Kuu inamlinda refa huku kila kukicha marefa wakiwa wanapewa vichapo.

5. Kocha sio Manager

Hili nalo inabidi liangaliwe kwa jicho pevu kwani ndio inaweza kua chanzo kikubwa sana cha timu zetu kufanya vibaya. Kwa nchi za wenzetu , mtu anapoteuliwa kua kocha anapewa pia u-manager wa timu kwa hiyo yeye ndio anakua juu ya mamlaka yote ya nani amsajili na kwa shilingi ngapi na nani amuache. lakini hapa bongo Kocha hana mamlaka kabisa, yeye analetewa tu majina ya wachezaji na anaambiwa awasajili. Hii ni kitu hatari sana na itazidi kuua mpira wetu hasa kwenye timu ya taifa ambapo unakuta kocha anachaguliwa timu ya taifa.

6. Mashabiki na uvumilivu

Yes , mlidhani nitawaacha. kuna kitu kinanisikitisha sana kuhusu mashabiki wa mpira wa Tanzania kwani ni wepesi wa kuhukumu na pia si wavumilivu. Timu imepewa kocha mpya, kafugwa mechi moja basi watu washaanza kuweka msimamo wa kumuondoa. Pengine tunapokosa uvumilivu ni uwanjani , unakuta watu wapo uwanjani mechi ikianza kwanza wanashangilia chenga , mtu kapigwa tobo , hivi hamuoni mechi za wenzetu watu wanaimba mwanzo mwisho hata timu ikiwa imepigwa goli 4 – 0 . sasa ngoja timu yao ifungwe hata goli moja hata hizo chenga hawatashangilia.

 

Mwisho nimnukuu rais wetu anayemaliza muda wake , Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake ya kufunga bunge ambapo alielezea mambo mbalimbali yanayohusu michezo kwa ujumla na jitihada zake alizozifanya katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake, kuna neno moja lilinikuna ambapo alisema haya, “Tusikate tamaa, tuendelee kujitahidi na iko siku tutafanikiwa mbele ya safari”.

 

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com