Vita ya ndugu wawili , Yanga VS KMKM


VIBONDE wa Gor Mahia, Yanga na KMKM wataumana saa chache zijazo katika muendelezo wa kuwania alama tatu muhimu. Yanga na KMKM, wanaalama sawa yaani 3 kila mmoja. Mapungufu yaliyojitokeza katika kikosi cha KMKM ni yaleyale ya kutokuwa na mshambuliaji mwenye kiwango cha kimataifa, mwenye ubora wa kupambana na walinzi wanaotumia akili kuunda ugumu kwenye safu yao ya ulinzi. Wanao washambuliaji wazuri ila hawawezi kukuahidi ushindi wanapokutana na safu ngumu ya ulinzi, hawana mshambuliaji mbunifu. Kwenye michezo mitatu waliyocheza, wamefunga mabao 3 tu. Huku mchezo mmoja pekee wakiwa wameshinda, ilikuwa dhidi ya Telecom. Hii inaonyesha kama wanahitaji ushindi basi wasiruhusu bao hata moja, huku wao wakifunga idadi yao ya kawaida. Sehemu nyingine ni makosa ya kizembe katika safu ya ulinzi, rejea katika mchezo dhidi ya Al Khortoum, bao la pili ni makosa ya mlinzi wa pembeni kuruhusu kupigwa ka krosi ilimfikia mfungaji kabla ya kuachia mkwaju mkali uliokwenda moja kwa moja na kutinga nyavuni. Idara ya ulinzi ya KMKM mpaka sasa imeruhusu kufungwa mabao 5 katika michezo 3, mchezo mmoja hawajaruhusu bao, hii ilikuwa dhidi ya Telecom ambao mpaka sasa ndio timu pekee iliyofungwa mabao mengi, mabao 9. Inaonyesha kwamba, kikosi chao kinaweza kufungika muda wowote.

Yanga-VS-KMKM-kagame-CECAFA-Cup-bongosoka

YANGA, hakuna shaka Salum Telela, anapocheza kama kiungo mkabaji yaani kiungo wa ulinzi, hutengeneza muunganiko mzuri kati ya idara ya kiungo na idara ulinzi. Huilinda vilivyo ngome yake isishambuliwe kirahisi. Pia hutengeneza umoja katika timu, ni rahisi kuona idara zote zikicheza kama timu kutafuta ushindi. Ubora wa Yanga, upo katika eneo la kiungo, mahala anapocheza Haruna Niyonzima na Salum Telela, hawa ni wasambazaji wa mipira kwenda mbele. Pia, upande wa pembeni mahala wanapocheza, Msuva au Mwashiuya na Kaseke. Kumeonekana kuleta matokeo chanya. Bao la tatu la Yanga dhidi ya Telecom, lilitokea huko. Mapungufu pekee ni kutoka mchezoni kwa wachezaji wakati mchezo ukiendelea, hii hutokana na maandalizi hafifu wanayopewa na kocha wao kabla ya mchezo, ni rahisi kuwaona wakipagawa wanapokutana na kitu tofauti mchezoni. Mfano, wapinzani wakitumia nguvu sana au wakishambulia kwa kasi. Sidhani kama Yanga, wanaweza kuruhusu kufungwa mbele ya mashabiki wao. Pia sijui kama KMKM watakubali kuruhusu kufungwa kirahisi. Mchezo kwa ujumla, utaamuliwa na maandalizi katika vyumba vya kubadilishia nguo, nidhamu ya mchezo kwa dakika zote 90, kutoruhusu makosa ya kizembe kutokea katika eneo la hatari hasa kwa KMKM kwani YANGA wanawatu wanaoweza kusababisha penalti. Vyote hivyo ni kwa kila mmoja wao. Mchezo wa mpira hutoa matokea yasiyotarajiwa, yasiyofikirika wala kudhaniwa. Huenda mkubwa akamuamkia mdogo au mdogo akalala bila chenji. Ahsanteni.

->Makala hii imeandikwa na  Halidi Abdulrahman.

 

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com