Yanga kusaka kikosi cha kwanza leo…


KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Van Pluijm amesema kwamba mpaka sasa hajapata kikosi cha kwanza na kila mchezaji hana budi kuthibitisha uwezo wake ili aingie kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Timu hiyo leo itashuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) ya Zanzibar katika mchezo, ambao kocha huyo atautumia kuwajaribu wachezaji wake katika kusaka kikosi cha kwanza. Pluijm, raia wa Uholanzi mwenye makazi yake Ghana aliliambia gazeti juzi kuwa mpaka sasa hajapata kikosi chake cha kwanza na kwamba hatapanga timu yake kwa kuangalia ukubwa wa jina la mchezaji bali uwezo wake uwanjani. Kikosi chote cha Yanga isipokuwa kiungo Haruna Niyonzima na beki Mbuyu Twite kinafanya mazoezi yake kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kujiandaa na mashindano ya Kombe la Kagame yatakayoanza kutimua vumbi Agosti 18.

Kikosi-cha-Yanga-Vs-SC-Villa

Akizungumzia kukosekana kwa nyota hao, Pluijm alisema kwamba Haruna Niyonzima yuko kwao Rwanda kwa matatizo ya kifamilia na Mbuyu Twite hajafanya mazoezi na wenzake tangia Ijumaa wiki iliyopita hali inayomfanya ashindwe kupata kikosi cha kwanza. “Mbuyu hajafanya mazoezi tangu Ijumaa na Niyonzima hajajiunga na wenzake. Siwezi na sitazungumzia kuhusu kikosi cha kwanza, kila mchezaji inabidi athibitishe uwezo wake,” alisema Pluijm. Yanga itacheza mchezo wa tatu wa kirafiki leo dhidi ya KMKM na Pluijm alisema kwamba mchezo huo utatoa fursa kwa mashabiki wa timu hiyo kuona viwango vya kiungo Joseph Zutta Tetteh kutoka Ghana na Donald Ngoma kutoka Zimbabwe. “Zutta anaweza kucheza kama beki lakini pia kama kiungo na Ngoma ni mshambuliaji, sitaki kuongea sana kuhusu wachezaji hawa, ila nitaacha viwango vyao viongee uwanjani,” alisema Pluijm ambaye ni muumini wa soka la kushambulia na burudani. Tayari mashabiki wa klabu hiyo wamekoshwa na viwango vya wachezaji Geofrey Mwashuiya, Deus Kaseke na Malimi Busungu kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Sports Club Villa ya Uganda na sasa wanasubiri kuwaona Donald Musoti kutoka Zimbabwe na Joseph Zuttah Tetteh kutoka Ghana.

Yanga-vs-SC-Villa-Kamara

Hata hivyo,Yanga katika mchezo huo ililazimishwa suluhu na timu hiyo ya Uganda katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Baadhi ya wachezaji ambao tayari walijaribiwa na kuonekana kufanya vizuri ni Deus Kaseke, Malimi Busungu na Geofrey Mwashiuya ambao walicheza kwa juhudi katika michezo miwili ya awali ya majaribio. Katika mchezo wa kwanza dhidi ya Friends Rangers, Busungu alifunga mabao mawili kati ya matatu yaliyofungwa siku hiyo na lingine likifungwa na Kpah Sherman. Katika mchezo wa kimataifa dhidi ya Sports klabu Villa ya Uganda uliochezwa kwenye uwanja wa taifa Kocha Pluijm alisema wachezaji hao walionesha kiwango cha hali ya juu.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com