Yanga yabeba Ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara


ILIKUWA furaha ya aina yake kwa mashabiki wa Yanga baada ya jana timu hiyo kukabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini ilikuwa huzuni kushindwa kuibuka na ushindi dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara na kutoka sare ya mabao 2-2.

Mchezo huo wa raundi ya 29 ulifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo hadi mapumziko Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 2-1. Ndanda ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 29 mfungaji akiwa Omari Mponda kwa njia ya penalti baada ya Raphael Amiri kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Thabani Kamusoko.

Hata hivyo dakika sita baadaye Simon Msuva aliisawazishia Yanga kutokana na pasi ya Geofrey Mwashiuya na dakika ya 40 Donald Ngoma aliifungia Yanga bao la pili, akimalizia mpira wa Haji Mwinyi.

Timu hizo zilishambuliana kwa zamu karibu muda mwingi wa kipindi cha pili, lakini umaliziaji ulikuwa tatizo kwa kila upande. Wakati mashabiki wakiamini pengine mchezo ungemalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi huo, huku furaha ikiongezeka kwa mashabiki wa klabu hiyo, mambo yalibadilika dakika ya 79 wakati Salum Minely aliposawazisha bao hilo akimalizia kazi ya Atupele Green na kuwafanya mashabiki wa Yanga kutulia kwa muda.

Wachezaji wa Yanga walijipanga na kushambulia kwa nguvu kutaka kuongeza bao la tatu, lakini Ndanda FC ilijipanga na kuhakikisha mchezo huo unamalizika kwa sare. Furaha ya mashabiki wa Yanga ilirejea kwa nguvu zaidi, baada ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba aliyekuwa mgeni rasmi katika mchezo huo kumkabidhi nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kombe la ubingwa wa ligi hiyo msimu wa 2015/16.

Ni taji la 26 katika historia ya klabu hiyo kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa ndiyo timu iliyochukua taji hilo mara nyingi, ikifuatiwa na mpinzani wake wa jadi Simba iliyotwaa ubingwa mara 18.

Yanga-Bingwa-ligi-kuu-Tanzania-Bara-Bongosoka-2

Yanga imekabidhiwa kombe hilo mapema kabla ya ligi kumalizika, baada ya katikati ya wiki hii kufikisha pointi 71 ambazo hakuna timu nyingine yoyote inaweza kuzifikia, ambapo kwa matokeo ya jana imefikisha pointi 72.

Yanga-Bingwa-ligi-kuu-Tanzania-Bara-Bongosoka

Azam FC inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 60 na ikishinda mechi zake mbili zilizosalia itafikisha pointi 66, wakati Simba yenye pointi 59 ambayo leo inacheza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani ina uwezo wa kufikisha pointi 65 ikishinda mechi zake mbili zilizosalia.

Mechi nyingine za ligi hiyo leo itakuwa kati Kagera Sugar ya Bukoba itaikaribisha Stand United ya Shinyanga Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Mbeya City.

Prisons itaikaribisha Toto Africans ya Mwanza Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Uwanja wa Mkwakwani, Tanga African Sports watakuwa wenyeji wa Azam FC. Ligi Kuu itamalizika Mei 21, mwaka huu, ambapo Mbeya City itacheza na Ndanda FC (Mbeya), Coastal Union na Prisons (Tanga), Simba SC na JKT Ruvu (Dar es Salaam), Toto Africans na Stand United (Mwanza), Azam FC na Mgambo JKT (Dar es Salaam), Kagera Sugar na Mwadui FC (Shinyanga), Mtibwa Sugar na African Sports (Morogoro) na Majimaji na Yanga SC (Songea).

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com