Yanga yaendelea kuifukuzia Simba , yaitandika Ndanda FC 2 – 1


Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara , Yanga wameendeleza kuonyesha kuwa hawako tayari kuachia kombe hili baada ya kuwatandika klabu ya  Ndanda FC  mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Yanga ndio ilikua ya kwanza kupata bao katika dakika ya sita ya mchezo kupitia kwa Pius Buswita baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Ndanda . Yanga waliongeza bao la pili katika dakika ya 29 ya mchezo kupitia kwa mchezaji wake , Hassan Kessy .

Yanga walipata Penati dakika ya 38 ya mchezo baada ya mchezaji wa Ndanda , John Tibar kuunawa mpira eneo la hatari  lakini kiungo Papy  Shitshimbi alikosa penalti hiyo iliyodakwa na kipa wa Ndanda Jeremia Kisubi.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika moja baadae Ndanda FC waliweza kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Nassor Kapama kwa shuti la kawaida akimalizia pasi ya Mrisho Ngassa ambaye aling’ara katika mchezo huo.

Ushindi wa leo ni wa kihistoria kwaYanga kwani ilikua haijawahi kuondoka na ushindi  kwenye ardhi ya Mtwara . Kabla ya mchezo wa leo ,  timu hizo zilikuwa zimecheza mechi tatu kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Yanga wanaendeleza ushindi wa sita  mfululizo kwenye ligi tangu iliposhinda 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting , 2-1 dhidi ya Azam FC, 2 – 0 dhidi ya  Lipuli ,  4-0 dhidi ya Njombe Mji na  4-1 dhidi ya  Majimaji .

Yanga inaendelea kushikilia nafasi ya pili ikiwa na pointi 40 nyuma ya wapinzani wao Simba wanaoendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 45.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com