Zifahamu vizuri timu 4 zilizopanda ligi kuu msimu huu…


Kuna mashabiki ambao hadi leo hajajua kwamba shirikisho la mpira Tanzania TFF , limeongeza timu 2 kwenye ligi kuu na sasa kuanzia msimu huu ligi itakua na timu 16 badala ya 14. Hii inaweza kua kicheko kwa timu nguli na kubwa  katika ligi hii kwasababu wanaweza kudhani kwamba wanaletewa timu zaidi ya kuzionea au inaweza kugeuka na kuwa mbogo kwani timu zilizopanda daraja msimu huu ni moto wa kuotea mbali na zimejitahidi kwenda sambamba katika usajili kama vilabu vingine. Timu zenyewe ni ;

Timu-zilizopanda-ligi-kuu-mwadui-majimaji-toto-africans-african-sports

African Sports ya Tanga

MWAKA 1988, mataji yote makubwa ya soka Tanzania yalikwenda Tanga, Coastal Union wakichukua ubingwa wa Bara, na African Sports wakabeba ubingwa wa Muungano.
Ubingwa wa Muungano ndiyo lilikuwa taji kubwa zaidi nchini wakati huo, michuano iliyoshirikisha timu za Bara na visiwini kumpata bingwa wa jumla wa nchi na pia wawakilishi wa michuano ya Afrika.  Pamoja na mambo kubadilika, lakini historia itabaki pale pale- kwamba African Sports walikuwa mabingwa wa nchi mwaka 1988. African sports ilianzishwa mwaka 1936 na maskani yake ni Barabara ya 12, Tanga, waasisi wake wakiwa marehemu Mohammed Msuo, Mwajitu, na Athumani Makalo pekee aliye hai kati ya waanzilishi. Africans Sports ilishuka daraja mwaka 1991 na tangu hapo imekuwa ikisota kurejea Ligi Kuu bila mafanikio hadi mwaka huu ambapo timu hiyo yenye historia yake itarejesha majeshi kwenye ligi kuu na kunauwezekano mkubwa ikaendelea kukaa katika ligi hii kutokana na kuwa na sapoti ya kutosha na pia udhamini walionao kutoka kampuni ya  Bin Slum Tyres Limited.

Mwadui FC ya shinyanga

kumbuka Timu hii ndio mabingwa wa ligi daraja la kwanza ambapo walitawazwa baada ya kuifunga  goli 1-0 timu ya African Sports ‘wana kimanumanu’ ya mkoani Tanga kwenye fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi. Kifedha wako vizuri na wako chini ya udhamini wa mgodi wa almasi wa Petra Diamonds -Wiliamson uliopo Mwadui Shinyanga.  Mwadui FC ni moja ya timu kongwe nchini, Ilicheza Ligi kuu kati ya miaka ya 70 na kisha kushuka kwenye miaka ya 80. Moja ya mafanikio ya timu hiyo ni kufika nusu fainali ya kusaka ubingwa wa Tanzania kwa kuitoa Yanga kwa mikwaju ya penalti. Kocha wao mwenye maneno mengi an uzoefu wa kutosha nchini, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ anategemea kuvipa wakati mgumu vilabu vingine katika kupigania kubaki ligi kuu.

 

Majimaji  ya Songea

Ni miongoni mwa timu ambazo zilikuwa tishio nchini katika miaka ya 1980 hadi iliposhuka daraja mwaka 2000. Kisha ikarejea tena mwaka 2009 na kushuka mwaka 2010. Mashabiki wengi wa soka nchini wanaikumbuka Maji Maji ya Songea maarufu kwa jina la Wanalizombe. Maji Maji ambayo ilianzishwa mwaka 1977 ilipata umaarufu mkubwa mwaka 1980, mwaka ambao timu hiyo ilipata nafasi ya kushiriki kwa mara ya kwanza Ligi Daraja la Kwanza ambayo kwa sasa ni Ligi Kuu. Majimaji ambao pia kipindi cha nyuma waliwahi kuchukua ubigwa wa muungano wanaleta changamoto kwenye ligi kuu msimu huu kutokana na kupigania kurudisha heshima waliokua nayo kipindi cha nyuma.

Toto Africans ya Mwanza

Toto Africans imepanda Ligi Kuu baada ya juhudi za muda mrefu. Klabu hiyo ilishuka daraja kutokana na ukata ulioikabili mwaka 2013. Kabla ya kushuka daraja miaka miwili iliyopita, Toto ilikuwa imecheza misimu sita mfululizo kwani ilikuwapo kwenye ligi tangu msimu wa 2007/08. Hivi sasa timu inaongeza utamu wa soka kwa Kanda ya Ziwa baada ya Kagera Sugar, Stand United na Mwadui nao kuwa na nafasi kwenye ligi. Tayari timu hiyo imeingia  makubaliano na wataalamu wa soka kutoka nchini Ujerumani kuhakikisha wanawawezesha kuwepo katika top 4 msimu huu.

Bongosoka imeungana na kampuni maarufu ya kubet ya 1XBet , Jiunge Hapa. Tufuate instagram , facebook na twitter. Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com